Wizara ya Maliasili na Utalii imewafunza wananchi
namna ya kubaini Asali isiyokuwa halisi ambayo
inadaiwa kutengezwa na wafanyabishara kwa
kutumia maji ya miwa yaliyochemshwa na
kubadilika kuwa sukari guru.
Akizungumza NIPASHE katika maonyesho ya
biashara ya 37 yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar e
Salaam jana, Ofisa nyuki na wakala wa huduma za misitu kutoka wizara hiyo,
Theresia Kamote, alisema kuna njia kadhaa za kuitambua asali iliyochakachuliwa.
Kamote alizitaja njia hizo kuwa ni pamoja na kuweka maji kwenye glasi na kisha
kumimina Asali na kwamba ikikaa chini ya glasi bila kuchanganyana na maji basi hiyo ni asilia na inakuwa haijachanganywa na chochote.
Alisema njia ya pili ni kuiweka Asali kwenye njiti ya kibiriti na kisha kuiwasha ikiwa
njiti hiyo itawaka basi Asali haijachakachuliwa kwa kuchanganywa na chochote lakini njiti ya kiberiti isipowaka inakuwa ni feki.
Aidha, Kamote aliongeza kuwa wizara yake imekuwa ikiwasisitiza wafanyabiashara
wa bidhaa hiyo kuwa waaminifu na kuwauzia wateja waoe bidhaa halisi na wale ambao bidhaa zao zinagundulika zimechakachuliwa ziharibiwa.
Aliongeza kuwa njia nyingine ni kuonja bidhaa hiyo na kwamba iliyokachuliwa kwa
kuchemsha inatoa harufu ya moshi tofauti na ambayo ni halisi.
“Wizara imekuwa ikitoa rai kwa wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kuwa waaminifu na
pale tunapogundua bidhaa yenyewe ni feki sisi kama wizara huwa tunaiharibu,”
alisisitiza Kamote.